Saturday, January 4, 2014

.........UPENDO !!!!


(Jua uhusiano kati ya UASI kwenye MAHUSIANO ya kijamii na UPENDO wako kwa Mungu)

Ukifuatilia nyakati katika maandiko utagundua kwamba tunaishi nyakati za mwisho. Tumekaribia mahali ambapo Yesu anarudi kulichukua Kanisa lake. Hakuna ajuaye ni karibu kiasi gani ila ni KARIBU. Yesu anasema yuko malangoni, anakuja.

Yesu alisema dalili ya nyakati za mwisho (Mathayo 24:3-13) na zinaonekana. Ila nataka niongelee MAASI. Huku mwisho wa nyakati tuliko tunaambiwa KUTAONGEZEKA MAASI na UPENDO wa wengi utapoa. Upendo ni kitu cha ajabu sana ambacho Mungu amewaumbia wanadamu. Mtu AKIPENDA ghafla! anakua mtu wa hatari maana huo UPENDO utamsukuma kufanya vitu bila kujali “sana” GHARAMA wala MUDA. Kwa mfano UPENDO wa mtu kwa Mungu utamsukuma huyo mtu kusimama kwa UAMINIFU mbele za Mungu hata kama anateseka na ataridhika na kila kitu kigumu na cha MAUMIVU alimradi asimtende Mungu dhambi. Sasa, UPENDO wa mtu huyu UKIPOA hutaamini vitu ataanza kufanya. Ghafla! visingizio vingi sana vinaibuka na sababu nyingi sana za MSINGI za kumkosea Mungu zinaibuka, ila ukifuatilia kinachotokea kwa huyu ndugu ni kitu kimoja tu UPENDO WAKE KWA MUNGU UMEPOA!

Sasa tunajua kabisa kwamba Mungu wetu ana NGUVU kuliko Ibilisi. Na hakuna siku ibilisi atakinga MSULI kwa Yesu akafanikiwa maana Yesu yuko juu sana katika UWEZA, sana sana ikiibuka vita atamtuma tu MIKAELI akamshughulikie huko na yeye akaendelea kumtizama BIBI ARUSI wake anayempenda sana ambaye ni KANISA. Ibilisi anachofanya hapa kwa wana wa Mungu ni KUONGEZA MAASI kati yao! USALITI katika mahusiano, biashara, familia, ndugu, huduma, nk. Huu usaliti unasababisha watu KUJERUHIWA ndani yao na UPENDO wao UNAPOA bila wao kujua! Wengi sana wamefika mahali pa gumu sana na wameweka SILAHA zao chini kwa sababu wamejeruhuwa na ADUI wakiwa KAZINI. Madhara yake yanapelekea KAZI yao kusimama shambani mwa Bwana, wamebaki KULAUMIANA na SHUHUDA MFU za watu waliowatendea mambo “mabaya” badala ya kushuhudia MATENDO makuu ya Mungu!

Watumishi wengi sana na wana wa Mungu wameacha zile SHUHUDA za “kuokoa” watu na Ibilisi ameanza kuwatumia kusambaza shuhuda KANDAMIZI za kurudisha watu nyuma! Ushuhuda ni habari NJEMA! Hili ndilo jina jingine la INJILI, habari njema kwa watu wote! Sasa, watu wengi sana wamewekeza kwenye habari MBAYA za watu na zimewavunja wengi sana moyo (hasa wachanga katika imani) na kuwajeruhi badala ya kuwajenga! Hayo MAASI ambayo yametokea, na WEWE mwana wa Mungu umejeruhiwa na umepata UCHUNGU na kwasababu hujashughulikia uchungu wako UMENAJISI wengi kanisani na madhara ya ule UASI “mmoja” umekua JANGA kubwa maana umesambaa na KUZIMISHA upendo wa WENGI kwa mara moja bila wewe kujua. Tunaonywa tuangalie “shina la UCHUNGU lisichipuke ndani yetu” maana UCHUNGU ndani ya mtu mmoja una uwezo wa kunajisi watu WENGI ambao hawakuhusika katika TUKIO lililosababisha huo uchungu. Chunga sana hili ENEO maana unaweza kujikuta umegeuka kuwa mtumishi wa Ibilisi kusambaza UCHUNGU bila kujua na ukamfanikishia Ibilisi kazi yake ya KUNAJISI watu!

Nitatoa mfano wa huduma ya Yesu. Wakati huduma ya INJILI inaendelea kwa kasi kubwa, Petro na wenzake “wako tayari kupigana kwa upanga kumtetea Yesu hadi kufa”, na ikafika mahali Petro anatoa upanga ALANI mwake kwa ajili ya kumlinda Yesu, na alijikuta anakata mtu sikio ghafla, aliona huyu jamaa anamsogelea Yesu. UPENDO kwa Bwana wake ukamsukuma “kupiga mtu”. Kabla Petro hajakaa sawa anaona YUDA, ambaye ni MTUMISHI mwenzake hapo pembeni anachukua RUSHWA, kabla hajakaa sawa anaona ANAMBUSU Yesu hadharani, kabla hajakaa sawa anaona Bwana wake AMESALITIWA LIVE na sasa ANASULUBIWA! Na aliyemsaliti ni MTUMISHI mwenzake ambaye wamefanya HUDUMA pamoja kwa takriban mika 3! Yesu alimwamini YUDA kiasi cha kumfanya MWEKA HAZINA wa HUDUMA yao. Leo machoni pa kila mmoja wao katika HUDUMA na wakiwa KAZINI anamsaliti Bwana wao! Hili jambo liliwasambaratisha wote wakatawanyika, sio kwa hofu tu ya wale waliokua wanamsulubu Yesu lakini pia ile hali ya UASI iliyojitokeza imeathiri UPENDO wao na WAKARUDI nyuma!

Kabla Petro hajakaa sawa anaulizwa “wewe si ulikua na huyu jamaa”, Petro anasema SIMJUI mtu huyu! Hataki hata kutaja jina la Yesu, safari hii anamwita “mtu huyu”! Mara tatu anamkana YESU hadharani! ila kilichotokea kabla ya hapo ni UASI mkuu na USALITI wa waziwazi! Wanafunzi walitawanyika kwa sababu “mchungaji wao amepigwa”. Petro akarudi zake KUVUA samaki ziwani, akaachana na BIASHARA ya Yesu maana UPENDO umepoa! Huyu ni Yule Petro ambaye alisema “hata wakikuacha wote mimi sitakuacha, niko tayari kufa kwa ajili yako, nk”. Sasa kimetokea nini? Upendo umepoa. Yesu alipofufuka akamtafuta tena Petro, akamuuliza “Petro UNANIPENDA?”, akarudia mara ya pili “Petro UNANIPENDA?” na mara ya tatu kurudia Petro AKALIA! Na akamwambia “Bwana unajua nakupenda…”. Ninachotaka uone hapa ni ile hali ya KUKATA TAMAA na KURUDI nyuma ya Petro baada ya VURUGU nyingi kutokea katika HUDUMA yao. Na YESU alikua ANAHUISHA ule UPENDO kati yao ambao ULIATHIRIKA. Hapo wakati Yesu anampa Petro kazi unaweza kujiuliza kwanini amuulize kwanza “unanipenda” ndio asema “LISHA KONDOO”, “CHUNGA KONDOO”, nk.? Sababu ya msingi hapa ni HUWEZI kufanya kazi ya MUNGU kama HUMPENDI! Jaribu uone halafu mbwa mwitu aje kama hujakimbia na kuacha KONDOO wanaliwa huko! Nakwambia mchungaji ANAYEPENDA kondoo zake “itamgharimu” maisha kwa kondoo hao. Sio mimi, ni maandiko yamesema.

Sasa katika maisha ya leo wengi wetu tumejeruhiwa sana na “watu” katika michakato mbalimbali ya maisha na kwa sababu UASI umeongezeka UPENDO wetu kwa Mungu na kwa “hao watu” umeathirika kwa viwango tofauti. Wengine WAMEACHA wokovu na wengine WAMERUDI nyuma. Sasa Ibilisi akifanikiwa kukurudisha nyuma, ukampa nafasi ya kurudi pale alikofukuzwa wakati unampokea Yesu, huwa anaongeza “idadi ya MAPEPO mara 7, tena wale waovu zaidi, na hali ya mtu huyu inakua mbaya kuliko ya mwanzo”! ili akifanikiwa “akuchinje” kabisa usije ukatubu!

Ukifahamu SIRI hii utagundua ni kwanini MTU akisalitiwa katika MAHUSIANO ni rahisi sana kurudi nyuma katika WOKOVU pia! Ule UASI una NGUVU ya KUPOOZA upendo wako kwa Mungu na kukumaliza kiroho USIPOANGALIA. Katika NDOA, HUDUMA, MAKANISANI, nk. kumekua na hiki kitu cha KUSALITIANA na kimeathiri kazi ya Mungu kwa kiwango kikubwa sana kwa sababu kimegusa eneo nyeti la UPENDO. Ni jambo la kusikitisha sana “mmoja” katika HUDUMA au NDOA anakua AGENT wa shetani “kwa muda” (bila kujua) kama ilivyokua kwa YUDA. Na kwa kipindi kifupi anatumika kufanya KITU ambacho kitasambaratisha HUDUMA au NDOA moja kwa moja. Ibilisi akimwachia huyu mtu (kwa maana ilikua kwa kitambo tu) akizinduka, anajuta! Ndio maana YUDA alikimbilia KITANZI na wala ile RUSHWA hakuila! Alisikia vibaya sana baada ya KUFANYA ule UASI na USALITI na akachukua ile HELA na kuirudisha kwa wenyewe! Too LATE! Yesu yuko msalabani saa hizo na huku huduma ishasambaratika WATUMISHI wenzake akina Petro nao “washaharibu” na akina Yohana na wenzake washatokomea kusikojulikana. Yesu alipofufuka alifanya kazi ya KUWAKUSANYA hawa wanafunzi wake kwa UPYA baada ya kusambaratika vibaya.

Angalia mambo ya kwanza uyape umuhimu wa kwanza. Watu wengi sana wako busy na HUDUMA na kusahau kwamba UPENDO ni msingi wa YOTE. Mungu havutiwi sana na hayo mambo kama HUMPENDI, na utakosa Ufalme wa Mungu usipojipanga pamoja na huduma yako kubwa nchi nzima au hata dunia nzima. Kumbuka (1 Wakorintho 13:1,2) “Tena nijapokuwa na UNABII, na kujua SIRI zote na MAARIFA yote, nijapokuwa na IMANI TIMILIFU kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina UPENDO, si kitu mimi. 2 Tena NIKITOA MALI ZANGU ZOTE kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu.” Shughulikia eneo lako la UPENDO wa KWANZA na Yesu. Fanya “toba” ya dhati ukikiri (kutaja kwa jina) pale “ulipoa anguka” maana unatakiwa UPAKUMBUKE na kumwambia Yesu, na kisha omba “maombi” yako ya dhati ili KUHUISHA ule UPENDO wa kwanza, na utaona mabadiliko na BARAKA zikimiminika kwako kwa namna ya tofauti.

Lengo la somo hili ni kukutahadharisha kuwa tuko nyakati za hatari. UASI ni mwingi na usipoangalia unaweza KUPOOZA UPENDO wako wa KWANZA! Na Yesu anasema na wewe akijua “umeuacha ule UPENDO wako wa kwanza”, ule ambao ulikuweka chini ukasoma Neno na kuomba na KUSHUHUDIA au kumtumikia Mungu katika ngazi mbali mbali. Naye anasema “kumbuka ni wapi ulipoanguka ukatubu”. Fanya HARAKA kwa sababu hizo njia za YUDA kweli zitakupa HELA, ila ni vipande 30 tu! Kumbuka thamani ya DAMU ya Yesu iliyokununua, FANYA uamuzi LEO kama UNAZIDI kumsaliti MWANA wa MUNGU au unamrudia. Mungu atusaidie kufanya maamuzi sahihi. NEEMA ya BWANA na iwe JUU yako tangu SASA na hata milele. AMEN.

Frank Philip.